Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU)
LENGO
Kutoa ushauri wa kitaaluma na huduma za habari, mawasiliano na midahalo na umma pamoja na vyombo vya habari
Kitengo kinaongozwa na;
Bw. Innocent P.M. Mungy
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (HGCU)
Barua pepe: Innocent.mungy@mawasiliano.go.tz
WASIFU
Bwana Mungy ni Mtaalamu wa Mahusiano ya Umma na Mawasiliano ya Kimkakati. Ni mkufunzi na mwezeshaji katika Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano ya Kimkakati. Ni Mwanataaluma aliyeidhinishwa na Taasisi ya Mahusiano ya Umma ya Uingereza (Chartered Institute of Public Relations – (MCIPR). Ni mwanachama wa Chama cha Kimataifa cha Mawasiliano ya Kimkakati ya Biashara (International Association of Business Communicators –(IABC). Bwana Mungy ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Maafisa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma Tanzania. Kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Bwana Mungy ana Shahada ya Uzamili (MA) katika Usimamizi wa Mawasiliano ya Kimkakati, Vyombo vya Habari na Ubunifu Habari kutoka Chuo Kikuu cha London Metropolitan, Shule ya Sanaa ya Sir John Cass. Bwana Mungy ana uzoefu wa muda mrefu katika usimamizi wa vyombo vya habari na mitandao ya mawasiliano. Amefanya kazi za Uhusiano na Mawasiliano nchini Tanzania na nje ya nchi kwa miaka 32. Amefanya kazi katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Alifanya kama Meneja Uhusiano Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) miaka ya 1990, Air Tanzania Corporation (ATC) miaka ya 1980. Pia alifanya kazi katika Serikali ya Uingereza kwenye Wizara ya Katiba na Sheria (Lord Chancelor’s Office) na Mahakama (Her Majesty’s Court Service) kama Mratibu wa Matukio ya Habari na Mawasiliano. Alirejea Tanzania mwaka 2006 na kuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Bw. Mungy ameandaa na kusimamia mikakati mbalimbali ya Mawasiliano nchini kama Uhamaji kutoka Analojia kwenda Dijitali, Kuzima Simu bandia nchini (counterfeit mobile phones switch off), Matumizi salama ya Mitandao ya Kijamii (Futa Delete Kabisa) nk. Bwana Mungy ni Mhadhiri anayefundisha katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini Tanzania na mshauri wa wataalamu kadhaa (mentor) wa Uhusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania. Bwana Mungy pia ni Mhadhiri wa Taasisi ya Uongozi Tanzania na Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere
MAJUKUMU YA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
(i) Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Mawasiliano;
(ii) Kuratibu utayarishaji na urushaji wa vipindi maalum vya TV na redio;
(iii) Kuratibu uzalishaji na usambazaji wa matoleo maarufu ya sera, kanuni na miongozo ya Wizara;
(iv) Kutayarisha na kutekeleza kampeni za Uhamasishaji Umma kuhusu matumizi na programu za huduma na miundombinu ya TEHAMA;
(v) Kupangilia ufanyikaji wa mahojiano ya kuandaa vipindi maalum vya TV na redio kuhusu maendeleo ya Sekta ya TEHAMA;
(vi) Kuandaa na kusimamia uzalishaji na usambazaji wa taarifa, elimu na mawasiliano kwa ajili ya wadau wa Wizara;
(vii) Kukuza ufahamu wa majukumu ya wizara, programu, miradi na sera kwa wadau na umma kwa ujumla;
(viii) Kuandaa maudhui na kuchapisha kwenye tovuti ya wizara na mitandao ya kijamii kwa ajili ya matumizi ya umma na wadau;
(ix) Kuanzisha na kufuatilia taratibu za kupata mrejesho kutoka kwa wadau na umma kwa ujumla;
(x) Kuchapisha na kusambaza Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa Wizara;
(xi) Kuratibu utoaji wa taarifa kupitia vyombo vya habari wakati viongozi wa Wizara, wabunge na wadau wa Wizara wanashiriki katika mikutano, semina, warsha, uzinduzi, kutembelea maeneo ya miradi inayotekelezwa na Wizara mijini na vijijini;
(xii) Kuratibu taarifa za Wizara kwa Vyombo vya Habari ili kuongeza uelewa na uwajibikaji kwa wananchi; na
(xiii) Kuratibu na kusimamia ufuatiliaji wa kila siku kwenye machapisho, majukwaa ya kielektroniki na mitandao ya kijamii kuhusu masuala yanayohusu TEHAMA.