Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Naibu Waziri Dkt. Mkama Awataka Maafisa Waandamizi Kuzingatia Maadili na Kujali Afya katika Utumishi wa Umma.


# Asema Afya ya Akili ni Msingi wa Utendaji Bora Kazini

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), amewataka Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Wizara hiyo pamoja na taasisi zake kuimarisha uongozi wa kimkakati, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, na kuweka kipaumbele katika ustawi wa afya zao ili kuongeza tija na ubora wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Dkt. Mkama alitoa wito huo alipokuwa akifunga mafunzo ya Viongozi na Maafisa Waandamizi yaliyofanyika tarehe 25 Februari 2026, Mtumba, jijini Dodoma. Aidha, aliongeza kuwa mafunzo hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora zitakazosaidia kuboresha utendaji kazi na kuimarisha uwajibikaji ndani ya taasisi za Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA.

Akizungumza kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma, Mhe. Dkt. Mkama alisisitiza umuhimu wa kuzingatia Itifaki, Kanuni na taratibu za Serikali ili kulinda hadhi ya taasisi na kuimarisha nidhamu ya kiuongozi.


Vile vile, alisema kuwa, uongozi wa kimkakati hauishii kwenye usimamizi wa shughuli za kila siku pekee, bali unahitaji dira iliyo wazi, upangaji wa maono mapana, na usimamizi madhubuti wa mabadiliko — hasa katika kipindi hiki ambacho sekta ya mawasiliano na TEHAMA inabadilika kwa kasi kubwa.

Dkt. Mkama alibainisha kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya Kikao cha Sekta ya Mawasiliano kitakachofanyika Februari 26, 2026, na kusisitiza kuwa maarifa yaliyopatikana yawasaidie washiriki kuboresha utendaji wao wa kila siku na kuongeza tija katika taasisi zao.

Aidha, aliwakumbusha washiriki kuhusu ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, magonjwa ya moyo na saratani, akihimiza umuhimu wa uchunguzi wa afya mara kwa mara, lishe bora na mazoezi ya mwili. Kuhusu afya ya akili, alieleza kuwa ni msingi wa utendaji bora kazini na kushauri kujenga utamaduni wa kuzungumza kwa uwazi, kusaidiana, na kutafuta ushauri wa kitaalamu inapohitajika.

Mhe. Dkt. Mkama alisema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika rasilimali watu, kwa kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea viongozi na watumishi wenye ujuzi, maadili, na afya njema.