Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tanzania Yaimarisha Dhamira ya Kuendeleza Akili Unde na Mageuzi ya Kidijitali


Na Mwandishi wetu, Shanghai China

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb), amewasili nchini China, kushiriki Mkutano wa Viongozi wa Juu wa Dunia wa Akili Unde (World Artificial Intelligence Conference) unaofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 20 Julai 2026.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Rais wa China, Mhe. Xi Jinping na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ambaye alipendekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa Akili Unde (Global AI Fund) utakaosaidia nchi zinazoendelea kupata rasilimali muhimu za kuendeshea vituo vya kutunzia taarifa na data za Akili Unde (AI Data Centre), mafunzo, msaada wa kiufundi na mengineyo.

 

Vilevile, mkutano huu   unawakutanisha viongozi wa serikali, watunga sera, wataalam, wabunifu wa teknolojia, wawakilishi wa sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na wadau mbalimbali wa sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka duniani kote.

 

Jukwaa hili linatoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, pamoja na kutafuta suluhisho za bunifu zitakazochochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali na mageuzi ya kidijitali kwa manufaa ya jamii.

 

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unadhihirisha dhamira ya Serikali ya Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya Akili Unde (AI), kujifunza mbinu bora za kimataifa na kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa kwa ajili ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali na maendeleo endelevu nchini.