Habari
JAMII MALIPO YAWEKA URAHISI NA USALAMA KATIKA MIAMALA YA WAFANYABIASHARA.
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Nzuguni – Dodoma
Wafanyabiashara wanaotembelea Banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, Dodoma, wamehamasishwa kutumia Mfumo wa Jamii Malipo kurahisisha miamala na kuongeza usalama wa fedha.
Akitoa elimu kwa wafanyabiashara hao, Afisa TEHAMA Mkuu, Bi. Asia Abdallah, amesema Jamii Malipo inawawezesha wafanyabiashara kufanya na kupokea malipo kwa njia ya kidijitali kwa haraka, usalama na urahisi, huku ikipunguza utegemezi wa fedha taslimu na hatari za wizi na upotevu wa fedha.
Amesema matumizi ya mfumo huo yanaongeza ufanisi wa biashara, uwazi katika miamala ya kifedha na ujumuishaji wa kifedha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukuza matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuchochea uchumi wa kidijitali nchini.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Bw. Charles, amesema elimu aliyopata kuhusu Jamii Malipo imemjengea uelewa wa manufaa ya kufanya miamala kwa njia ya kidijitali na kumshawishi kuanza kutumia mfumo huo katika shughuli zake za biashara.
“Nitawashauri wateja wangu wafanye malipo kwa njia ya kidijitali ili kuchangia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,” amesema Bw. Charles.
Wizara inaendelea kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za kidijitali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali, kuboresha huduma na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
