Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI KAIRUKI AZINDUA PROGRAMU YA MIKOPO KWA KAMPUNI CHANGA ZA TEHAMA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amezindua rasmi Programu ya Uwezeshaji wa Mikopo kwa Kampuni Changa za TEHAMA, yenye lengo la kuwawezesha vijana na wabunifu kupata mitaji ya kuendeleza bidhaa, huduma na biashara zao za kidijitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo, Oktoba 02, 2026, katika Ofisi za Wizara, Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, Waziri Kairuki amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 kupitia Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji kwa ajili ya kusaidia kampuni changa zinazomilikiwa na vijana kupata mitaji ya kukuza bunifu zao.

Ameongeza kuwa mikopo hiyo itatolewa katika madaraja matatu, ambapo mkopo mdogo utakuwa kati ya Shilingi milioni 1 hadi milioni 25, mkopo wa kati zaidi ya milioni 25 hadi milioni 50, na mkopo mkubwa zaidi ya milioni 50 hadi milioni 100, kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.

Katika hafla hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeshuhudia hatua ya makabidhiano ya fedha kwa Benki ya Azania kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo, sambamba na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara na Benki hiyo.

Waziri Kairuki amesema programu hiyo inalenga kuhakikisha mtaji unaopatikana unachochea ubunifu, uzalishaji wa bidhaa na huduma, ukuaji wa kampuni, uundaji wa ajira na upanuzi wa masoko, akisisitiza kuwa fedha hizo ni kichocheo cha kukuza kampuni changa na kuongeza mchango wa sekta ya TEHAMA katika uchumi wa Tanzania.


####