Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATUMISHI WAPYA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI NA KUWA WACHAPAKAZI


Na Mwandishi Wetu, Singida

Watumishi wapya wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, kufanya kazi kwa uadilifu na kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya Serikali na Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Fatuma Kalovya akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi ya Awali kwa Waajiriwa Wapya wa Wizara yanayofanyika tarehe 20 Oktoba 2026 Mkoani Singida.

Bi. Kalovya amewapongeza watumishi hao kwa kupata ajira na kuwataka kutambua kuwa ajira ni dhamana inayohitaji bidii, nidhamu, utii, uadilifu na utoaji wa huduma kwa wananchi bila upendeleo.

Aidha, amewasisitiza watumishi hao kutumia mafunzo hayo kuelewa vyema Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, maadili na uwajibikaji, huduma bora kwa mteja, usalama wa Serikali pamoja na usimamizi wa kumbukumbu na mawasiliano ya kiofisi. Mafunzo hayo pia yanalenga kuwajengea uelewa kuhusu haki na wajibu wao katika utumishi wa umma.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo waajiriwa wapya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kutoa mchango wenye tija katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini.