Habari
MKAMA: TEHAMA NI CHACHU YA KUBORESHA HUDUMA ZA POSTA NCHINI
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi, tija na ubora wa huduma za Posta nchini, hususan katika kipindi hiki cha mageuzi ya kidijitali duniani.
Amesema hayo Novemba 26, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenda Shirika la Posta Tanzania, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya teknolojia na kuboresha utoaji wa huduma za Posta.
Dkt. Mkama amesema Mashirika ya Posta Duniani yanabadilika kutoka taasisi zinazojikita katika usafirishaji wa barua pekee na kuwa vituo vya huduma za kidijitali, biashara mtandao, huduma za kifedha na huduma za Serikali mtandao. Ameeleza kuwa Shirika la Posta Tanzania lina nafasi ya kipekee kutumia mtandao wake unaofika kuanzia ngazi ya vijiji hadi kitaifa kuwaunganisha wananchi na huduma hizo.
Aidha, amesema uwekezaji huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kisasa na shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia. Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, huduma za Serikali mtandao na ujuzi wa kidijitali ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Ameeleza kuwa hatua hiyo pia inaunga mkono Sera ya Taifa ya Posta pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan ujenzi wa miundombinu na ubunifu, kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma na kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi. Ameipongeza UCSAF kwa ushirikiano wake na Shirika la Posta Tanzania katika kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kuboresha maisha ya wananchi.
Dkt. Mkama amelitaka Shirika la Posta Tanzania kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi ili kuongeza thamani ya huduma na kuimarisha imani ya wananchi, huku UCSAF ikiendelea kusimamia miradi inayogusa maisha ya wananchi na kuhakikisha uwekezaji unaleta matokeo yanayopimika. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Sekta ya Posta na Mawasiliano inakuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
