Habari
WATOA HUDUMA ZA MALAZI, CHAKULA NA UTALII WAJENGEWA UWEZO WA KUTUMIA MIFUMO YA KIDIJITALI KUNUFAIKA NA AFCON 2027
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam
Serikali imewajengea uwezo watoa huduma za malazi, chakula na utalii kutumia mifumo ya kidijitali ili kuboresha huduma, kutangaza biashara zao na kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kujitokeza wakati wa mashindano ya AFCON 2027.
Hatua hiyo imefanyika kupitia mafunzo yaliyotolewa jijini Dar es Salaam yakilenga kuwajengea washiriki uwezo wa kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) na Jamii Apps katika kurahisisha shughuli za biashara na utoaji wa huduma kidijitali.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Justine Mwaipopo, amesema kupitia NaPA, watoa huduma wataweza kusajili biashara zao ili zitambulike na kufikika kwa urahisi kwa kutumia teknolojia.
Ameeleza kuwa Jamii Apps inaunganisha huduma mbalimbali zikiwemo Jamii Pay, Jamii Wezesha, Jamii Food, Jamii Pass, Jamii Shop, My Ticket na Visit Tanzania. Kupitia Jamii Pass, mtumiaji anaweza kupata huduma kwa kutumia akaunti moja, huku Jamii Pay ikiwezesha malipo ya kielektroniki, ununuzi mtandaoni na usimamizi wa oda.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Michael Nyahinga, amesema mfumo wa JamiiWezesha umeandaliwa kuratibu, kutambua na kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo katika sekta isiyo rasmi kuunganishwa na fursa za Masoko, Mikopo, Mafunzo, Bima ya Afya na hifadhi ya jamii.
Aidha amesema kuwa mfumo wa NaPA utawawezesha watoa huduma za utalii kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini kupitia jukwaa moja, hatua itakayosaidia kuongeza idadi ya watalii na mapato ya Taifa.
Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gift Kyando Enock, amesema AFCON ni tukio la kimataifa linalohitaji maandalizi ya kutosha na huduma bora. Hivyo amewataka watoa huduma kusajili biashara zao kupitia NaPA na kutumia Jamii Apps na kufanya biashara na malipo kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wageni watakaotembelea nchini.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha maandalizi ya tukio hilo yanaenda sambamba na uboreshaji wa huduma.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuwaandaa wananchi kutumia teknolojia katika kuboresha biashara zao na kunufaika na fursa zitakazotokana na AFCON 2027.
