Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAIPA KIPAUMBELE MIUNDOMBINU YA KIDIJITALI KAMA NGUZO YA UKUAJI WA AFRIKA.


Na Mwandishi Wetu, WMTH - Singapore.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ametoa wito wa kuifanya miundombinu ya kidijitali kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya Afrika, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Asia katika kuharakisha uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.

Wito huo umetolewa wakati wa Mazungumzo ya Uwekezaji wa Miundombinu kati ya Afrika na Singapore (Africa-Singapore Infrastructure Investment Dialogue), yaliyofanyika nchini Singapore na kuwakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji, taasisi za fedha na viongozi wa biashara kwa lengo la kujadili fursa za kuunganisha vipaumbele vya maendeleo ya miundombinu barani Afrika na mitaji, teknolojia pamoja na utaalamu kutoka Singapore na Asia.

Waziri Kairuki amesema Teknolojia na Mawasiliano vimekuwa sehemu muhimu ya miundombinu ya sekta mbalimbali, ikiwemo nishati, gridi za umeme, bandari na usafirishaji. Alisisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu ya kidijitali yanapaswa kupewa kipaumbele sawa na miundombinu mingine ya kawaida ili kuharakisha ukuaji wa uchumi wa Afrika.

Ameleza kuwa kuimarisha ubia kati ya serikali na sekta binafsi za Afrika na Asia kutasaidia kuvutia uwekezaji, kuharakisha ujenzi wa miundombinu na kufungua fursa mpya za kiuchumi katika mnyororo mzima wa thamani wa miundombinu. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Taifa wa Singapore, Bw. Alvin Tan, alieleza dhamira ya nchi hiyo ya kuimarisha ushirikiano na Afrika, hususan katika miundombinu, nishati, usafirishaji, uchumi wa kidijitali, teknolojia za fedha na malipo ya kuvuka mipaka. 

Pia ametaja majadiliano yanayoendelea kuhusu Mkataba wa Biashara Huria kati ya Singapore na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao una umuhimu kwa Tanzania kama mwanachama wa jumuiya hiyo.

Mazungumzo hayo pia yalijikita katika kutafuta njia bunifu za ufadhili wa miradi na kuimarisha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), kupitia mkutano wa meza ya duara uliowakutanisha wawakilishi wa serikali, benki, wawekezaji na wadhamini wa miradi. Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Invest Africa, Bi. Chantelé Carrington, alisema mazungumzo hayo ni hatua muhimu katika kuunganisha mitaji, utaalamu na teknolojia ya Singapore na Kusini-Mashariki mwa Asia na mahitaji ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika.

Katika kuendeleza ushirikiano huo, Singapore inatarajiwa kushika Uenyekiti wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) mwaka 2027, huku Jukwaa la Biashara kati ya Afrika na Singapore (Africa-Singapore Business Forum) likipangwa kufanyika Julai 2027. Matukio hayo yanatarajiwa kutoa fursa zaidi za kuendeleza ushirikiano wa uwekezaji na biashara kati ya kanda hizo mbili.