Habari
TANZANIA NA ESTONIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA TEKNOLOJIA ZA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu, Doha, Qatar
Tanzania na Estonia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari. Ushirikiano huo utajikita katika maendeleo ya huduma za kielektroniki (e-Services), ujenzi wa mifumo ya kidijitali na kubadilishana utaalamu kwa lengo la kukuza uchumi wa kidijitali.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Wawakilishi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU PP-26) unaoendelea jijini Doha. Mazungumzo hayo yaliwakutanisha Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, na Waziri wa Sheria na Masuala ya Kidijitali wa Estonia, Mhe. Liisa Pakosta.
Katika mazungumzo hayo, Tanzania ilieleza nia yake ya kuendeleza miradi ya pamoja na Estonia itakayolenga kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi.
Waziri Kairuki aliipongeza Estonia kwa kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika katika maendeleo ya TEHAMA. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya kidijitali na kupunguza pengo la kidijitali, hasa wakati huu ambapo teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Unde (AI), zinakua kwa kasi kubwa.
Kwa upande wake, Mhe. Pakosta alisema Estonia imekubali pendekezo la Tanzania la kuanzisha ushirikiano wa vitendo kwa kubainisha mradi maalumu wa pamoja, hususan katika eneo la huduma za kielektroniki na uendelezaji wa mifumo ya kidijitali.
