Habari
NaPA KUCHOCHEA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUELEKEA AFCON 2027
Na Mwandishi wetu – WMTH Arusha.
Watoa huduma za malazi, chakula na utalii wameshiriki mafunzo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi (NaPA), yaliyoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yaliyolenga kuwasaidia kutumia fursa za kidijitali kukuza biashara zao kuelekea AFCON 2027.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Ndugu Mosses Pesha amewataka wafanyabiashara kujisajili kwenye mfumo huo ili biashara zao zitambulike na kuonekana kidijitali hatua hiyo itarahisishia wageni kutafuta huduma na kufika kwenye maeneo husika.
Aidha, ameongeza kuwa mifumo kama Jamii Apps itawezesha biashara za kidijitali na malipo ya kielektroniki, pamoja na JamiiWezesha, inayolenga kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo na Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutumia fursa za kidigitali.
Amesisitiza kuwa kupitia anwani sahihi zinazopatikana kidijitali, wageni wanaweza kuelekezwa kwenye maeneo ya malazi, chakula na utalii kwa urahisi zaidi. Mfumo huo pia utasaidia wajasiriamali kujitangaza na kuwafikia wateja wengi zaidi kidijitali huku wakiboresha uchumi kutokana na shughuli zao.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 pamoja na nchi za Kenya na Uganda, Majiji ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar yakiwa ndio maeneo ambayo yatatumika.
