Habari
BUNGE LARIDHIA AZIMIO LA TANZANIA KUJIUNGA NA MKATABA WA USALAMA ANGAMTANDAO (MKATABA WA MALABO)
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Bungeni Dodoma.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia Azimio la mapendekezo ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Usalama wa Angamtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa mwaka 2014, maarufu kama Mkataba wa Malabo.
Azimio hilo limewasilishwa Bungeni na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ambaye amewasilisha mapendekezo ya Tanzania kujiunga na mkataba huo unaolenga kuimarisha usalama wa anga ya kidijitali na ulinzi wa taarifa binafsi.
Kuridhia azimio hilo ni hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha usalama wa anga ya kidijitali nchini, kulinda taarifa binafsi za wananchi pamoja na kujenga mazingira salama na ya kuaminika katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Usalama wa mtandao ni jambo muhimu sana katika ustawi wa taifa lolote duniani, na kwa kadri matumizi ya mtandao yanavyoongezeka, ndivyo ambavyo matishio ya usalama wa mtandao na makosa yanayofanyika kupitia mtandao yanavyozidi kuongezeka,” alisema Waziri Kairuki.
Mkataba huo unaweka mfumo wa pamoja kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kukabiliana na uhalifu wa kimtandao, kuimarisha mifumo ya usalama wa taarifa, pamoja na kuweka misingi ya kisheria ya ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi sahihi ya taarifa binafsi.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb) alisema kamati inaunga mkono kuridhiwa kwa Mkataba wa Malabo, nakusisitiza kuwa hatua hiyo itaipa Tanzania fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika masuala ya usalama wa mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi na biashara ya kielektroniki.
Kuridhia Mkataba wa Malabo kunaonesha dhamira ya Tanzania ya kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuimarisha usimamizi wa masuala ya usalama wa mtandao na ulinzi wa taarifa binafsi, ikiwa ni sehemu ya kujenga uchumi wa kidijitali ulio salama, jumuishi na endelevu.
