Habari
SERIKALI YASAJILI ANWANI ZA MAKAZI MILIONI 13
Shirika la Posta lapongezwa kwa makusanyo ya Shillingi Bilioni 51.9
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amesema Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) ni nyenzo muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuimarisha usalama, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Waziri Kairuki ameyasema hayo tarehe 20 Oktoba, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) na utendaji wa Shirika la Posta Tanzania mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Bungeni, jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa, Hadi Oktoba 18, 2026, anwani za makazi 13,004,796 zilikuwa zimesajiliwa, huku mfumo huo ukiwa umeunganishwa na mifumo 36 ya Serikali, ikiwemo TAUSI, e-Ardhi na NIDA.
Akitoa taarifa kuhusu Shirika la Posta Tanzania, Waziri Kairuki amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Shirika lilikusanya mapato ya Shilingi bilioni 51.9, kutoka bilioni 44.2 mwaka uliotangulia. Pia, lilipata faida kabla ya kodi ya Shilingi bilioni 8.4, sawa na asilimia 421 ya lengo lililopangwa.
Kupitia maboresho hayo, Serikali imewezesha ununuzi wa magari 12 yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.2 na bajaji 50 za umeme zenye thamani ya Shilingi milioni 250. Shirika pia limepokea vyeti vya kimataifa vya usalama vya Umoja wa Posta Duniani (UPU) na kuboresha mifumo ya kidijitali ya ufuatiliaji wa mapato na mizigo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb.), ameishauri Serikali kuendelea kusimamia utendaji wa Shirika la Posta Tanzania ili kuongeza ufanisi na kuimarisha maslahi ya watumishi wake.
