Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI KAIRUKI ATOA MAELEKEZO KUBORESHA PROGRAMU YA MIKOPO KWA KAMPUNI CHANGA ZA TEHAMA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), ametoa maelekezo sita ya kuboresha utekelezaji wa Programu ya Uwezeshaji wa Mikopo kwa Kampuni Changa za TEHAMA, ikiwemo kuharakisha uchambuzi na utoaji wa mikopo, kupanua fursa za masoko na kuweka mfumo wa kupima matokeo ya programu hiyo.

Waziri Kairuki ametoa maelekezo hayo tarehe 2 Oktoba, 2026 jijini Dodoma na kuelekeza kuwa wabunifu na kampuni changa zinazolengwa na programu hiyo kujisajili katika Mfumo wa Jamii Hunt, utakaotumika kuwatambua walengwa na kupokea maombi ya mikopo. Huku akisisitiza kuwa maombi yaliyokamilika yashughulikiwe kwa ufanisi na kwa wakati.

Wakati huo huo, Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya TEHAMA (ICTC) kukamilisha mwongozo wa kuwezesha kampuni changa za TEHAMA kushiriki katika zabuni za Serikali na kuwasilisha suala hilo kwa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma kwa hatua stahiki. Hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za masoko na kuwawezesha kampuni hizo kushiriki katika biashara zinazotokana na mahitaji ya Serikali.

Katika kupima ufanisi wa programu, Waziri Kairuki amezielekeza Wizara, Tume ya TEHAMA na Benki ya Azania kuweka mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaozingatia ukuaji wa kampuni, ajira zilizozalishwa, ongezeko la mauzo na mapato, masoko yaliyofikiwa, bidhaa na huduma mpya pamoja na urejeshaji wa mikopo.

Vilevile, amewataka wabunifu kuanzisha umoja rasmi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, ili kurahisisha uwakilishi wao, utambuzi wa changamoto na uwasilishaji wa mahitaji yao. Ameagiza pia kuandaliwa kwa mpango wa elimu kwa umma kuhusu vigezo na taratibu za maombi, wajibu wa wanufaika na manufaa ya programu hiyo.

Waziri Kairuki amesisitiza kuwa kampuni zitakazonufaika zinapaswa kutumia mikopo kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kukuza biashara, kutafuta masoko ndani na nje ya nchi na kuchangia maendeleo ya sekta ya TEHAMA Tanzania.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kampuni changa, huku akisisitiza kuwa mikopo hiyo inapaswa kutumika kama kichocheo cha ubunifu, biashara, ajira, mapato na ongezeko la thamani katika uchumi wa Tanzania.


####