Habari
SERIKALI, BENKI YA DUNIA YATATHMINI UTEKELEZAJI WA MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu – WMTH
Wataalamu kutoka Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia wamekutana jijini Dar es Salaam kufanya tathmini ya utekelezaji na maendeleo ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), inayolenga kuimarisha mabadiliko ya kidijitali nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na teknolojia kwa wananchi.
Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa chini ya uratibu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo tarehe 14 Septemba, 2026, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ni sehemu muhimu ya juhudi za Serikali katika kuharakisha mabadiliko ya kidijitali nchini.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unalenga kuchochea upatikanaji na uboreshaji wa huduma za umma, kuongeza tija, kukuza ubunifu, kuibua fursa za ajira na kuwezesha uwekezaji katika sekta ya TEHAMA.
Bw. Kiwango ameihakikishia Benki ya Dunia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Timu ya Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine, ili kuhakikisha mradi huo unaleta matokeo yanayoonekana na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Bakari Mwamgugu, amezitaka taasisi zinazotekeleza mradi huo kuongeza kasi ya kukamilisha shughuli zilizobaki, pamoja na kuhakikisha uwekezaji uliofanyika unatumika kikamilifu na kwa uendelevu.
Amesema Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 150, ulioanza kutekelezwa mwaka 2021, unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2026.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo ni ujenzi wa minara 437 ya mawasiliano, uboreshaji wa minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda teknolojia za intaneti zenye kasi zaidi, uanzishwaji wa Vituo nane vya Ubunifu wa TEHAMA pamoja na vituo viwili vya ukarabati wa vifaa vya TEHAMA.
Aidha, amesema mradi umechangia kuimarisha miundombinu ya kidijitali ya Serikali kupitia upatikanaji wa uwezo wa intaneti ya kimataifa wa Gbps 60, mifumo ya kubadilishana taarifa ya Serikali, ikiwemo Jamii X-Change na Zan X-Change, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA kwa taasisi za umma.
Viongozi hao wamezitaka taasisi zinazotekeleza mradi huo kutumia fursa ya tathmini hiyo kutatua changamoto zilizopo, kukamilisha kwa wakati shughuli zilizobaki na kuweka mikakati madhubuti ya uendelevu wa uwekezaji uliofanyika.
Wamesema hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha matokeo ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali yanaendelea kutumika kwa ufanisi na kuchangia kuboresha huduma za kidijitali pamoja na kuongeza manufaa kwa wananchi.
