Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KAIRUKI: TUZO ZA TEHAMA ZICHOCHEE BUNIFU NA KUINUA UCHUMI WA KIDIJITALI.


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb), amesema Tuzo za TEHAMA 2026 ni kichocheo cha kutambua na kuhamasisha wabunifu, wajasiriamali, wawekezaji na vijana wanaotumia teknolojia kutatua changamoto na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika Usiku wa Tuzo za TEHAMA 2026, Waziri Kairuki amesema TEHAMA imekuwa muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, elimu, madini na fedha. Amesema jumla ya maombi 345 yalipokelewa katika makundi 14 yenye vipengele vidogo 46, huku ukaguzi wa mchakato wa uteuzi uliofanywa na Deloitte ukilenga kuhakikisha uwazi na uadilifu.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo Mkongo wa Taifa na minara ya mawasiliano, huku akiwataka wabunifu kutumia fursa hizo kuendeleza mifumo na bunifu zinazoboresha huduma na kuchochea uchumi wa kidijitali.

Aidha, Waziri Kairuki ameitaka Tume ya TEHAMA kuongeza ushiriki wa wadau na kulifanya tukio hilo kuwa la Kitaifa zaidi, pamoja na kuweka mikakati ya kukuza na kutangaza bunifu zinazoshinda hadi kutambulika kimataifa. Amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kuimarisha nafasi yake katika mapinduzi ya kidijitali barani Afrika.