Habari
TANZANIA YAONESHA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA AKILI UNDE (AI) KATIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA WAICO 2026
Na Mwandishi Wetu Shanghai - China.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amewasilisha mafanikio ya Tanzania katika maendeleo na usimamizi wa Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) wakati akihutubia Mkutano wa Viongozi wa Juu wa Dunia kuhusu masuala ya AI tarehe 18 Julai, 2026, jijini Shanghai, China.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Kairuki alisema ya kwamba wamekutana kwa sababu Akili Unde ni teknolojia ambayo dunia haijawahi kuwa nayo hapo awali na hivyo haijawahi kuweka mikakati Madhubuti ya Menejimenti yake. Ni teknolojia inayojifunza, inayovuka mipaka ya nchi moja mpaka nyingine, na ambayo inaweza kuathiri maisha ya watu wengi ambao hata hawakuwahi kuichagua au kuishi nayo kwa namna moja ama nyingine. Alisisitiza ya kuwa menejimenti ya AI haiwezi kufanywa na nchi moja, inahitaji ushirikiano wa nchi kadhaa. Kunahitajika mfumo Mpya, Imara na Madhubuti unaojengwa kwa ushirikiano wa pamoja na nchi nyingine, na hivyo Tanzania iko tayari kuunga mkono maazimio ya mkutano yatakayotolewa kwa lengo kuwezesha kuwa na menejimenti bora ya AI.
Tanzania inaunga mkono juhudi za kimataifa za kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa AI unaozingatia mshikamano wa kimataifa, maadili, usalama na matumizi yenye manufaa kwa watu wote. Alisisitiza kuwa AI ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo endelevu, hususan katika sekta za kilimo, afya, elimu, utawala wa kidijitali, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi wa kidijitali.
Akili unde si teknolojia ya kesho au baadae tena, bali imekuwa sehemu ya miundombinu ya maisha yetu ya leo na ya sasa. Kwa nchi inayoendelea, huu si mjadala wa kinadharia, kwa mfano Tanzania, Akili Unde si anasa tena bali ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo katika Nyanja mbalimbali kama vile kilimo, afya, elimu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kukuza uchumi shirikishi unaowanufaisha wananchi wote kwa ujumla wake.
Mwaka uliopita tulizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Pamoja na Mambo mengine, inaelezea JAMII AI inayohusu mfumo wa lugha ya Kiswahili (Large Language Model) kwa kuwa Kiswahili inaweza kuwafikia zaidi ya watu milioni 200. Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika tangu mwaka 2022, pia ni lugha mojawapo ya kazi ya Umoja wa Mataifa. Hivyo, ndivyo tunavyohakikisha kuwa uchumi wetu wa kidijitali unakuwa shirikishi na unamfikia kila mwananchi popote alipo.
Vilevile, tunaendelea kujenga miundombinu itakayowezesha mabadiliko ya kidijitali tunayoyahitaji. Tunaendelea kuimarisha uti wa mgongo wa uchumi wa kidijitali kupitia vituo vinne vya mikongo ya bahari vilivyopo Tanzania pamoja na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Data za Akili Unde. Kituo hiki kitahakikisha kuwa Tanzania haitakuwa tena chanzo cha kusambaza tu taarifa ghafi kwa nchi nyingine za Afrika na nje ya Afrika. Kwa kuhifadhi data zetu nchini, wabunifu na watafiti wa Tanzania na Afrika wataweza kujenga na kufundisha mifumo ya akili unde kwa kutumia data zetu, kwa kutumia nishati zetu endelevu, ikiwemo umeme wa maji na nishati ya jotoardhi.
Kwa kuwa thamani ya miundombinu hutegemea watu wanaoitumia, Taasisi yetu mpya ya Teknolojia ya Kidijitali iliyopo jijini Dodoma itawaandaa wabunifu wa kesho kwa kuwapatia ujuzi unaohitajika katika enzi hizi za Akili Unde, sambamba na mikakati ya akili unde ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mustakabali wa Akili Unde si simulizi linalosubiri kuandikwa; ni mfumo ambao tunapaswa kuujenga pamoja, kuanzia leo. Hatuwezi kuruhusu kasi ya ubunifu kuzidi maadili yetu, wala kuruhusu hofu kutuzuia kutumia fursa kubwa ambazo teknolojia hii inaleta kwa maendeleo endelevu.
Tujitolee kujenga mfumo wa utawala wa akili unde unaokwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia yenyewe, mfumo unaolinda utu wa binadamu, unaoziba pengo la tofauti za kijiografia na kisiasa, na unaohakikisha kuwa nguvu ya akili unde inatumika kwa manufaa ya pamoja ya wanadamu wote.
