Habari
TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHWA KWA MIUNDOMBINU YA TEHAMA
*TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHWA KWA MIUNDOMBINU YA TEHAMA*
Na Mwandishi Wetu, Bahamas.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ustahimilivu wa mitandao ya mawasiliano na TEHAMA ili kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kupatikana wakati wa majanga na changamoto mbalimbali.
Akizungumza katika Mjadala wa Kimaudhui kuhusu Ustahimilivu wa Mawasiliano na TEHAMA wakati wa Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Sera za Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (WTPF-26), uliofanyika jijini Nassau, The Bahamas, Waziri Kairuki amesema ustahimilivu wa mawasiliano si suala la kiufundi pekee, bali ni sehemu ya usalama wa taifa, mwendelezo wa shughuli za kiuchumi na usalama wa wananchi.
Amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuimarisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao sasa una zaidi ya kilomita 15,000, kuunganisha mifumo ya nyaya za chini ya bahari na nchi jirani, pamoja na kuanzisha Mpango wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura.
Aidha, amesema Serikali imeanza kutambua na kusajili Miundombinu Muhimu ya TEHAMA, huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na timu ya kitaifa ya kukabiliana na dharura za mtandao, TZ-CERT, zikiimarisha ufuatiliaji na ushirikishwaji wa miundombinu.
Waziri Kairuki amezitaka nchi Wanachama kuongeza uwekezaji katika njia mbadala za mawasiliano, nishati ya akiba, vituo salama vya kuhifadhi taarifa na satelaiti, huku akisisitiza ushirikiano wa kimataifa katika tahadhari za mapema, kukabiliana na vitisho vya mtandao, ukarabati wa nyaya za mawasiliano na uhamishaji wa teknolojia na ujuzi.
