Habari
TANZANIA YAAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA KOREA KATIKA TEKNOLOJIA ZA KIDIJITALI NA AKILI UNDE
Na Mwandishi Wetu, Seoul
Akizungumza katika Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika (KOAFEC) uliofanyika Seoul, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ametaja Taasisi ya Teknolojia ya Kidijitali (DTI) iliyopo Dodoma kuwa ni mfano dhahiri wa matokeo ambayo yanaweza kupatikana kupitia ushirikiano kati ya Tanzania na Korea.
Taasisi hiyo inajengwa kwa ufadhili wa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 167.37 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea (EDCF), na itakuwa kituo cha umahiri katika tafiti za Akili Unde (AI), ubunifu na mafunzo ya ujuzi wa kidijitali.
Waziri Kairuki ameeleza vipaumbele vitatu kwa awamu inayofuata ya ushirikiano huo ambavyo ni kuongezwa kwa ufadhili wenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa (data centres) pamoja na miundombinu ya Akili Unde, uhamishaji wa teknolojia na ujuzi kupitia programu za kubadilishana wataalamu, pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya kampuni za teknolojia za Korea na kampuni changa za teknolojia (startups) barani Afrika.
Amesema ajenda ya Tanzania ya maendeleo ya kidijitali imejikita katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kidijitali jumuishi unaopunguza pengo la kidijitali kati ya maeneo ya mijini na vijijini, pamoja na kuunda fursa zaidi kwa wanawake na vijana.
Waziri Kairuki amesisitiza tena dhamira ya Tanzania ya kuhakikisha matokeo ya mkutano huo yanatafsiriwa kuwa uwekezaji wenye tija na matokeo halisi kwa manufaa ya wananchi
