Habari
TANZANIA NA HUAWEI WATIA SAINI MAKUBALIANO YA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA UCHUMI WA KIDIJITALI NA UBUNIFU.
Na Mwandishi Wetu Shanghai - China
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Kampuni ya Huawei Technologies Tanzania Limited zimetia saini Hati ya Makubaliano yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maendeleo ya uchumi, ubunifu na mageuzi ya kidijitali.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Shanghai, China na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Tiger Liu kwa niaba ya Kampuni ya Huawei, huku yakishuhudiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), na Rais wa Huawei wa Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Pever Gao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kairuki alisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimkakati utakaosaidia kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya Tanzania ya uchumi wa kidijitali sambamba na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alieleza kuwa maeneo ya ushirikiano yatakayotekelezwa kupitia MOU hiyo ni pamoja na kuendeleza miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), matumizi ya Akili Unde, kuimarisha miundombinu ya huduma za umma kidijitali, kujenga na kuendeleza wataalamu wa ndani wa TEHAMA, pamoja na kukuza uzalishaji, uunganishaji, matengenezo na ukarabati wa vifaa vya kidijitali.
Mhe. Kairuki alibainisha kuwa Serikali inatarajia ushirikiano huo kuleta matokeo yenye tija ikiwemo kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji, kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa njia za kidijitali, kuwajengea vijana ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, kuimarisha mifumo ya ubunifu na kusaidia ukuaji wa kampuni changa za teknolojia.
Kwa upande wake, Rais wa Huawei wa Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Gao, alisema Huawei itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Tanzania katika safari ya mageuzi ya kidijitali, akieleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na Serikali kwa zaidi ya miaka 20 katika kupanua mawasiliano, kujenga miundombinu ya TEHAMA, vituo vya kuhifadhi taarifa (Data Centers) na kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya TEHAMA.
Alisisitiza kuwa makubaliano hayo yataongeza ushirikiano katika maeneo ya Akili Unde (AI), miundombinu ya TEHAMA, ukuzaji wa vipaji na ubunifu wa teknolojia ili kuisaidia Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
