Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano Yanategemea Uwajibikaji na Uongozi Thabiti – Waziri Kairuki


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mtumba, Dodoma

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesisitiza umuhimu wa weledi, maadili na ubora wa huduma katika kuimarisha misingi na maendeleo ya sekta ya Mawasiliano nchini.

 

Akizungumza katika kikao kazi kati ya Wizara, Bodi na taasisi zilizo chino ya Wizara kilichofanyika tarehe 27 Februari 2026, Waziri Kairuki aliwataka Viongozi wa Bodi na Menejimenti kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika utendaji wa kazi ili wananchi wapate huduma bora na zenye tija.

Waziri Kairuki alisisitiza kuwa misingi imara ya maendeleo inajengwa kupitia uongozi thabiti na usimamizi bora wa rasilimali za umma. Aidha, aliagiza kuongeza kasi ya uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu, hususan katika maeneo yasiyo na huduma muhimu, ili kupanua wigo wa upatikanaji na kupunguza pengo kati ya mijini na vijijini.

 

Waziri Kairuki alisisitiza umuhimu wa kampeni za elimu kwa umma na vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo na kujilinda dhidi ya changamoto za kidijitali.

 

Aidha, aliongeza kuwa ni muhimu kukuza na kutumia wataalamu wazawa, kuwezesha mafunzo na kuongeza ujuzi wa watumishi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuhakikisha uendelevu wa miradi ya kimkakati.

 

Waziri Kairuki alihimiza ushirikiano aliwataka katika kufanya kazi kwa pamoja na ubunifu na uwajibikaji wa hali ya juu, huku akibainisha kuwa utekelezaji madhubuti wa maelekezo hayo utaimarisha huduma, kuongeza imani ya wananchi na kuchochea kasi ya maendeleo ya sekta ya mawasiliano na taifa kwa ujumla.