Habari
Waziri Kairuki: Serikali Kujenga Ushirikiano Imara na Sekta Binafsi Kukuza Uchumi wa Kidijitali
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mtumba, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angela Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameongoza kikao kazi kati ya Wizara na wadau wa sekta binafsi kilichofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Februari 26, 2026.
Kikao hicho kimekusudia kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa kidijitali.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kuwa Wizara inaendelea kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Anga za Juu, ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa tarehe 8 Februari 2022, kuhusu Serikali kumiliki satelaiti yake kwa ajili ya kutatua changamoto za mawasiliano nchini.

Amesema programu hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa Taifa katika matumizi ya Teknolojia za Anga ili kuboresha mawasiliano, kusaidia sekta za uzalishaji, kuimarisha usalama na usimamizi wa rasilimali, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji na ubunifu.
“Ni matarajio yetu kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi, programu hii itachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa kidijitali na maendeleo ya Taifa kwa ujumla,” amesema Waziri Kairuki.
Aidha, Waziri Kairuki ameeleza kuwa Wizara inaendelea kuimarisha Ulinzi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA (Critical Information Infrastructure – CII) kwa kuzingatia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na miongozo mbalimbali ya kutambua, kusajili na kulinda miundombinu hiyo.
Amesema mwongozo na amri ya kutangaza Miundombinu Muhimu ya TEHAMA iko katika hatua za mwisho za uridhiwaji, hatua ambayo itatatua changamoto ya muda mrefu ya kukosekana kwa mfumo wa kisheria wa ulinzi wa miundombinu hiyo.

Waziri Kairuki ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwajibika katika kuilinda na kuendeleza miundombinu hiyo kwa kushirikiana na Wizara, akisisitiza kuwa ni jukumu la pamoja kuhakikisha usalama, uimara na uendelevu wa miundombinu hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Akiendelea kueleza mikakati ya Wizara, Waziri Kairuki amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni chachu ya ubunifu, uwekezaji na ajira katika sekta ya teknolojia.
Ameeleza kuwa Wizara inashirikiana na wadau katika uandaaji wa Akaunti ya Upimaji wa Uchumi wa Kidijitali (DESA), ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi za mchango wa sekta ya TEHAMA katika pato la Taifa.
Waziri Kairuki amewataka watoa huduma za mawasiliano kuhakikisha wanatumia miundombinu iliyopo kwa pamoja (Co-location), na pia kutumia miundombinu iliyojengwa na Serikali kupitia mfumo wa National Roaming ili kupunguza urudufu wa rasilimali na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana nchi nzima.
Aidha, amesisitiza dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 hakuna eneo nchini litakalokuwa halina huduma za mawasiliano.

“Kwa umoja wetu, tuelekeze nguvu kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 hakuna sehemu itakayokosa mawasiliano (‘Zero Spot’). Nina imani tutafanikiwa kwa kishindo,” amesema Waziri Kairuki.
Kwa upande mwingine, Waziri Kairuki amebainisha kuwa Wizara inaandaa Mwongozo wa Ujenzi Nadhifu wa Miundombinu ya Mawasiliano (National Deployment Guideline for ICT Infrastructure) ili kuhakikisha ujenzi wa miundombinu unazingatia ubora, usalama na matumizi ya pamoja, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama.
Pia, Waziri Kairuki ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Wizara katika kufanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa mfano wa mji wa kisasa unaotumia TEHAMA (Smart City).
Amesema Wizara itatoa utaratibu wa namna wadau wanaweza kushiriki katika hatua hiyo muhimu, akisisitiza kuwa ni fursa ya kihistoria kwa Tanzania kuonesha uwezo wake katika matumizi ya teknolojia bunifu za mijini.
Akihitimisha kikao hicho, Waziri Kairuki amesisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari kwa kushirikiana na sekta binafsi, ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari inakuwa nguzo ya maendeleo ya Taifa letu — salama, bunifu, na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Waziri Kairuki.
