Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ZOEZI LA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI MBEYA KUANZA NYUMBA KWA NYUMBA ALHAMISI


Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza kuwa kuanzia Alhamisi, Septemba 25, zoezi la uhakiki na uhuishaji wa taarifa za anwani za makazi katika Jiji la Mbeya litaanza rasmi kwa kupita nyumba kwa nyumba.

Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 23, 2025 na Afisa TEHAMA na mtaalam wa Mfumo wa Anwani za Makazi wa Wizara hiyo, Bi. Rehema Mwinjuma, wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loleza iliyopo jijini humo.

Bi. Mwinjuma amesema zoezi hilo la uhakiki linalenga kuboresha taarifa zote za anwani ili mfumo wa kidijitali wa NaPA uwe na taarifa sahihi, zitakaorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kuanzia tarehe 25 tutaanza kupita nyumba kwa nyumba kuhakiki na kuhuisha taarifa za anwani, zenye makosa zitarekebishwa, na wale ambao hawakuwahi kupatiwa anwani awali watapewa anwani zao na kuingizwa kwenye mfumo wa NaPA,” amesema Bi. Rehema.

Ameeleza kuwa zoezi hilo linatanguliwa na mafunzo ya siku mbili yatakayotolewa kwa watendaji wa mitaa, kata na wenyeviti ili kuhakikisha kila timu ina uelewa wa kutosha kabla ya kuanza kazi rasmi.

Ameongeza kuwa, takwimu za awali zinaonesha kuwa, mfumo wa NaPA ulikusanya zaidi ya anwani 481,000 katika Jiji la Mbeya. Hata hivyo, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka baada ya zoezi la uhakiki kwa kuyafikia maeneo ambayo hayakufikiwa hapo awali.

Bi. Mwinjuma ametoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa watendaji, kwa kutoa taarifa sahihi zitakazohitajika ili kusasisha taarifa na kuimarisha mfumo wa anwani za makazi nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi na usahihi wa taarifa, na hatimaye kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Kama mtu hatakutwa nyumbani, tunaomba aache taarifa muhimu kama namba ya kiwanja, jina la mmiliki, namba ya simu, NIDA na taarifa za wategemezi kama mume, mke, watoto, ndugu au wapangaji,” amesisitiza Bi. Rehema.