Habari
Tanzania, Kuimarisha Ushirikiano katika uendelezaji wa matumizi ya Akili Unde
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameshiriki Mkutano Mkuu wa masuala ya Akili Unde nchini India ulioanza tarehe 18 Februari, 2026.
Katika Mkutano huo, Waziri Kairuki amesilisha taarifa ya utayari wa nchi ya Tanzania kushirikiana kuhakikisha kuwa matumizi ya Akili Unde yanakuwa endelevu, imara na ya kiubunifu huku yakizingatia uimarishaji wa mazingira na matumizi ya nishati bora.
Waziri Kairuki amesema kuwa moja ya vipaumbele katika kuendeleza matumizi ya Akili Unde nchini ni kuwekeza katika Ujenzi wa Vituo vya Kuhifadhia Data, kuimarisha mashirikiano na Sekta Binafsi ikiwemo watafiti na wabunifu kuhakikisha kuwa matumizi ya Akili Unde yanaleta tija nchini.
Kabla ya Mkutano huu, Wataalam kutoka Tanzania wameshiriki katika vikao kazi vya Mkutano huu kujadili namna ambavyo nchi itahakikisha kuwa matumizi ya Akili Unde yanakuwa jumuishi na endelevu.
Pembezoni mwa Mkutano huo, Waziri Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na Waheshimiwa Mawaziri kutoka nchi mbalimbali, wawekezaji na makampuni makubwa yanayoongoza katika Akili Unde kwa lengo la kuona namna gani Tanzania itakavyonufaika na fursa mbalimbali kupitia wadau hawa.
Mkutano Mkuu wa Masuala ya Akili Unde ulioanza tarehe 18 Februari, 2026 nchini India unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 20 Februari, 2026.
