Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

JUKWAA LA PAMOJA LA SATELAITI LA SADC 2026 LAENDELEA JIJINI DAR ES SALAAM


Jukwaa la Pamoja la Satelaiti la SADC 2026 limeendelea jijini Dar es Salaam tarehe 17 Februari, 2026 ambapo wadau wa sekta ya mawasiliano kutoka nchi zote 12 wanachama wa SADC, pamoja na taasisi mbalimbali za kikanda wameendelea kujadili maendeleo ya teknolojia za satelaiti na matumizi ya anga za juu katika kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali katika nchi za SADC.

Tanzania, ikiwa mwenyeji wa jukwaa hili kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za kikanda za kukuza teknolojia za mawasiliano na kuhakikisha nchi wanachama zinanufaika na fursa za anga kwa ajili ya maendeleo endelevu. 

Wajumbe kutoka Taasisi za Umma za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na Sekta Binafsi wamewakilisha nchi katika majadiliano ya kiufundi na ya kisera yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika teknolojia za satelaiti.

Katika siku ya pili ya mkutano huo, washiriki wamejadili baadhi ya ajenda ikiwemo Mpango Kazi wa Utekelezaji wa kuongeza uwezo wa ziada kwenye Mtandao wa Pamoja wa Satelaiti wa SADC, Taarifa ya Mapendekezo ya Ukubwa na Muundo wa Antena za Vituo vya Ardhi, pamoja na Rasimu ya Mpango wa Biashara wa Mtandao wa Pamoja wa Satelaiti wa nchi za SADC.

Kupitia ushiriki wake katika jukwaa hili, Tanzania inaendelea kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha mawasiliano na teknolojia katika ukanda wa Afrika ya Kusini, na kama mshiriki muhimu katika juhudi za kuimarisha uchumi wa kidijitali wa kikanda.