Habari
Serikali na Benki ya Dunia Watathmini Hatua za Mradi wa Tanzania ya Kidijitali
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Arusha
Wataalamu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya Taifa ya TEHAMA (ICT Commission), Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-Government Authority - eGA), Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu ya Zanzibar, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), pamoja na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia, wamekutana jijini Arusha kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (Digital Tanzania Project - DTP).
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Salome Kessy, amesema tathmini hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa, na matokeo yanayotarajiwa kwa Wananchi.
Amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha uwekezaji unaofanywa kupitia mradi huo unaleta mageuzi ya kweli katika utoaji wa huduma za umma kwa njia ya kidijitali.
Kikao hicho kililenga kupitia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mkopo wa masharti nafuu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya TEHAMA na kukuza huduma za kidijitali nchini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Bakari Mwamgugu alisema kuwa tathmini hiyo inalenga kupima hatua zilizofikiwa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano, upatikanaji wa huduma za Serikali Mtandao, pamoja na kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika taasisi za umma.
Aidha, kikao hicho pia kilitoa fursa kwa wataalamu kujadili changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo masuala ya uratibu kati ya taasisi, kasi ya utekelezaji wa baadhi ya vipengele, na umuhimu wa kuendelea kujenga uwezo kwa wataalamu wa TEHAMA ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa wakati.
Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano na teknolojia ya habari, kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa njia ya mtandao, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali—hatua itakayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
