Habari
WIZARA YAZINDUA MAFUNZO YA NDANI KWA WATAALAM WA MRADI WA MAWASILIANO VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua Mafunzo ya Ndani ya Nchi kwa Wataalam wanaosimamia Mradi wa Mawasiliano Vijijini ili kuwajengea uwezo wa kiufundi katika usimamizi wa mitandao ya simu vijijini, uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano, pamoja na utatuzi wa changamoto zinazohusu huduma za simu na intaneti.
Akifungua rasmi mafunzo hayo leo Septemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Salome Kessy, amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, awe mjini au kijijini, anapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano ikiwemo simu, intaneti, na redio kupitia TBC Taifa.
Aidha, aliwashukuru wataalam hao kutoka taasisi za TTCL, TBC na UCSAF kwa mchango wao mkubwa katika utekelezaji wa mradi huo na kupongeza wataalam hao wa ndani kwa mshikamano wao katika kuhakikisha mradi unafanikiwa.
“Jukumu mlilopewa si dogo, ninyi ni sehemu ya historia ya mageuzi ya mawasiliano nchini Tanzania,” alisema Bi. Kessy, akisisitiza kuwa maeneo ya vijijini ambayo hayakuwa na huduma za mawasiliano sasa yanaenda kuunganishwa na fursa za maendeleo.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku, amesema Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano Vijijini unaendelea kutekelezwa kwa kasi ambapo unahusisha ujenzi wa jumla ya minara 636, kati yake 621 ya simu na 15 ya redio, ukiwa na thamani ya dola za Marekani milioni 108.5 kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.
Amesema hadi kufikia tarehe 29 Septemba 2025, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 56, ambapo minara ya simu 261 imejengwa na kati yake 130 tayari inatoa huduma, ujenzi wa minara ya redio unaendelea, na ufungaji wa mfumo wa miundombinu mikuu ya mawasiliano katika vituo vya TTCL Dar es Salaam na Dodoma umekamilika kwa asilimia 90.
Aidha, Bw. Munaku ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, ambapo wataalam 72 kutoka taasisi mbalimbali wameshajengewa uwezo nchini China katika maeneo ya mbalimbali ya usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano.
“Hivi leo tunazindua mafunzo ya ndani ya nchi ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 07 Novemba 2025, yakihusisha wataalam 140, lengo kuu likiwa ni kuongeza ujuzi na weledi wa usimamizi na uendeshaji wa miundombinu hii muhimu ya mawasiliano vijijini,” alisema Bw. Munaku.