Habari
Kamati ya Bunge Yaipongeza TTCL, Yataka Maboresho ya Haraka Miundombinu na Masoko ya Mawasiliano.
Na Mwandishi wetu - WMTH Dar es salaam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Seleman Kakoso, leo Machi 17, 2026 imefanya ziara katika Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukagua na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mawasiliano nchini. Kamati hiyo ilipokelewa na uongozi wa Wizara ya Mawasiliano pamoja na menejimenti ya TTCL wakiongozwa na Waziri wa wizara hiyo Mhe. Angellah Jasmine Kairuki.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Mhe. Angellah Jasmine Kairuki alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya mawasiliano inaendelea kukua kwa kasi, akibainisha kuwa maoni yote yaliyotolewa na kamati yatazingatiwa kabla ya kuwasilishwa kwa randama ya bajeti tarehe 27 ya mwezi huu. Alisisitiza kuwa maboresho ya miundombinu ni kipaumbele cha wizara yake.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alifafanua kuhusu mpango wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhi data (Data Center) jijini Dodoma, akieleza kuwa upembuzi yakinifu umekamilika na mashauriano na Wizara ya Fedha yanaendelea. Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha ujao ili kuimarisha usalama na uhifadhi wa taarifa za serikali.
Aidha, alibainisha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 30 kinatarajiwa kutumika katika kuboresha vifaa vya Data Center kwa muda mfupi. Wizara tayari imetoa ridhaa kwa TTCL kupata dola za Marekani milioni 3.8 kwa ajili ya kuimarisha mitambo, huku kiasi kingine kikitarajiwa kutolewa na serikali ili kuboresha zaidi miundombinu hiyo muhimu.
Kuhusu upanuzi wa huduma, Waziri Kairuki alisema serikali itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa zaidi ili kuongeza ufanisi wa mawasiliano nchini. Alitaja pia mradi wa mawasiliano vijijini unaogharimiwa kwa mkopo wa takriban dola milioni 108, ambao unahusisha ujenzi wa minara ya simu na uboreshaji wa huduma za mawasiliano hususan maeneo ya mipakani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema shirika linaendelea kupanua wigo wa huduma zake kupitia makubaliano ya ushirikiano (roaming agreements) na makampuni kama Airtel na Yas, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa mtandao. Aliongeza kuwa TTCL inaendelea kuwekeza katika teknolojia ya fiber optic pamoja na mifumo ya point-to-point ili kufikia maeneo mengi zaidi nchini.
Mwenyekiti wa Kamati, Mhe.Seleman Kakoso, aliipongeza wizara na TTCL kwa juhudi wanazofanya lakini akasisitiza umuhimu wa kuboresha zaidi masoko ya huduma za shirika hilo ili kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa ruzuku ya serikali. Pia alisisitiza umuhimu wa kuboresha masilahi ya wafanyakazi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa kuhitimisha, kamati hiyo iliitaka serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ikiwemo kupeleka mkongo wa taifa katika nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hatua itakayosaidia kukuza mapato ya taifa. Kamati pia ilipendekeza kuandaliwa kwa semina maalum ya wabunge kuhusu mfumo wa “Jamii Pay” ili kuongeza uelewa na matumizi yake nchini.
