Habari
SERIKALI YASISITIZA USHIRIKISHWAJI WA WADAU UANDAAJI WA MPANGO WA KITAIFA WA MIUNDOMBINU YA TEHAMA
Na Mwandishi Wetu, WMTH, Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ndugu Hawwah Ibrahim Mbaye, amesema kuwa ili kuimarisha maendeleo ya kidijitali ni muhimu kuhakikisha kuwa kunakuwa na mipango itakayowezesha upatikanaji wa miundombinu bora ya TEHAMA inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Ameyasema hayo leo tarehe 12 Machi, 2026 wakati akifungua Kikao cha Wadau cha kupata uelewa kuhusu Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Miundombinu ya TEHAMA na Mwongozo wa Ujenzi wa Miundombinu ya TEHAMA nchini.
Naibu Katibu Mkuu Mbaye ameongeza kuwa ushiriki wa wadau mbalimbali katika kutoa maoni yao ni muhimu ili kuhakikisha mpango na mwongozo huo unakuwa jumuishi, unaotekelezeka na unaochochea maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa Sekta ya Umma na Binafsi katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
