Habari
USIMAMIZI MADHUBUTI WA DATA ZA KIELEKRONIKI KULETA MAGEUZI KUFIKIA MAENDELEO YA DIRA YA TAIFA 2050
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohamed Mashaka, amesema kuwa katika zama za mapinduzi ya kidijitali, Data imeibuka kuwa moja ya rasilimali muhimu na yenye thamani kubwa kwa maendeleo ya nchi.
Amesema hayo tarehe 12 Machi, 2026 wakati wa Kikao Kazi cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu uandaaji wa Mkakati Madhubuti wa Kitaifa wa Usimamizi wa Data za Kielektroniki kilichofanyika jijini Dodoma.
Bw. Mashaka amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa wakati nchi inaelekea kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, usimamizi bora wa data za kielektroniki si suala la kiufundi pekee, bali ni jambo muhimu linalogusa haki za faragha za wananchi, ustawi wa uchumi na uwezo wa serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Bw. Mashaka ameeleza kuwa data za kielektroniki zimekuwa sehemu muhimu katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na Sekta Binafsi, ambapo zinatumika katika kufanya maamuzi sahihi, kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameongezea kuwa kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia, dunia imeingia katika hatua ya kuzalisha kiasi kikubwa cha data, jambo linalochochea mapinduzi ya kidijitali. Hata hivyo, ili kunufaika ipasavyo na mapinduzi hayo, upo umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya usimamizi na matumizi sahihi ya data.
Bw. Mashaka amesema kuwa pamoja na fursa zilizopo katika matumizi ya data za kielektroniki, bado kuna changamoto mbalimbali zinazohusiana na usimamizi wa data, ikiwemo kutokuwepo kwa mikakati iliyo wazi ya usimamizi wa data katika baadhi ya taasisi pamoja na kutokuwiana kwa sera na taratibu zinazohusu matumizi na ubadilishanaji wa data.
Kikao Kazi hicho kimebainisha kuwa usimamizi mzuri wa data za kielektroniki ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali na kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na kujenga Tanzania yenye uchumi wa kidijitali unaotumia teknolojia na TEHAMA katika kuharakisha maendeleo ya Taifa.
