Habari
WIZARA YATOA MAFUNZO YA USALAMA MTANDAONI KWA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA BUNGE, DODOMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu ya Usalama Mtandaoni kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge ya mkoani Dodoma, ikilenga kujenga uelewa kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii na teknolojia za kidijiti.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Oktoba 8, 2025, yamelenga kuwawezesha wanafunzi kujilinda dhidi ya vitendo hatarishi mtandaoni, hasa wakati wa vipindi vya likizo ambapo matumizi ya simu za mkononi huongezeka miongoni mwa vijana.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Wakili Mwandamizi wa Serikali kutoka Wizara hiyo, Bw. Moris Cyprian Sarara, aliwasisitiza wanafunzi hao kuwa waangalifu na mienendo yao katika ulimwengu wa kidijiti, akiwasihi kuwa ulinzi wa faragha zao ni ngao muhimu kwao kama watoto wa kike katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia.
Kwa upande wake, Esther Gembe, mwanafunzi wa kidato cha tano aliyewakilisha wenzake, aliishukuru Wizara kwa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewasaidia kuelewa namna ya kujilinda mtandaoni na kutumia teknolojia kwa manufaa.