Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YAKETI NA SEKTA BINAFSI KUTATHMINI NA KUPANGA MAENDELEO YA SEKTA


Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari imefanya kikao cha tathmini ya utendaji wa Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA kwa lengo la kufanya mapitio ya maeneo yaliyofanyiwa utekelezaji na kuweka mipango ya maeneo yatakayofanyiwa utekelezaji kupitia bajeti inayoandaliwa ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Kikao hicho kilichofanyika lMachi 18 na 19, 2024 jijini Arusha kimehusisha Menejimenti ya Wizara, Wajumbe wa Bodi na Wakuu wa Taasisi chini ya Wizara hiyo; Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar; Mamlaka ya Serikali Mtandao (JMT na SMZ); NIDA; Wadau na Watoa huduma wa Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA kutoka Sekta binafsi.

Akihutubia wajumbe wa kikao hicho Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imepanga kuihusisha sekta binafsi katika mipango ya utekelezaji na bajeti kwa lengo la kushirikiana kusukuma gurudumu la maendeleo.

“Tumebadilisha namna Serikali inavyosimamia na kufanya kazi na Sekta binafsi, na hapa tunatekeleza zile R nne za Rais Samia ambazo ni Maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya na tumeonesha inawezekana na sekta binafsi zinafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na Serikali”, amezungumza Waziri Nnauye

Akizungumzia miongoni mwa mafanikio yaliyoigusa Wizara na Serikali ni pamoja na kumalizika kwa majadiliano na mafanikio yaliyopatikana kupitia Mkataba wa mashirikiano (MoU) baina ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano.

Aidha ametoa rai kwa watoa huduma kuendelea kushirikiana na Serikali katika uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano lakini pia Sekta binafsi kushirikiana katika utoaji wa huduma, akitolea mfano mnara mmoja wa mawasiliano unaweza kutumiwa na watoa huduma wote badala ya kila mtoa huduma kujenga mnara wake katika eneo moja

“Umefika wakati tuwe tunapata huduma za Roaming za mitandao ya ndani yan chi ili mnara wa mtandao wowote nitakaokuwa nao karibu niweze kupata huduma kupitia Roaming bila kubadili laini ya simu”, amesisitiza Waziri Nnauye

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa amesema kuwa kikao hicho kimetumika kujadili kwa pamoja kuhusu mipango na vipaumbele vya Serikali ili vikatafsiriwe vema na sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara hiyo.

Amesema kuwa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 wa Wizara hiyo utaonesha maeneo yatakayotekelezwa na Serikali na maeneo yatakayotekelezwa kwa ushirikiano na sekta binafsi katika sekta zote tatu za Habari, Mawasiliano na TEHAMA.

Akizungumza kwa niaba ya Mhe Selemani Kakoso, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki na mjumbe wa kamati hiyo amesema wao kama wabunge na kama Kamati wanatambua mchango mkubwa wa sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo wataendelea kusapoti jitihana zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi.