Habari
WIZARA YAENDELEZA HAMASA YA UHAKIKI WA TAARIFA ZA ANWANI NA MAKAZI

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kuhamasisha wananchi kuhakiki taarifa zao za Anwani za Makazi kwa ajili ya kurahisisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 23, 2022.
Kwa nyakati tofauti wananchi waliojitokeza kuhakiki anwani zao wameeleza kuwa zoezi hilo ni la manufaa kwani linawasaidia wao kuweza kujua taarifa zao za makazi endapo zipo sahihi kwenye mfumo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi, Mhandisi Jampyon Mbugi alieleza kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi ni msingi wa utambuzi wa maeneo ya makazi, vituo vinavyotoa huduma za jamii na maeneo ya biashara.
Ameeleza kuwa ili mwananchi aweze kuhakiki anwani yake ya makazi, lazima awe anafahamu namba ya nyumba, barabara, mtaa/kitongoji na kata anayoishi. Taarifa hizo, licha ya kuhitajika wakati wa Sensa ya Watu na Makazi, zitakuwa ni taarifa za kusaidia Serikali kupanga na kuboresha mipango ya maendeleo inayokidhi mahitaji kwa kulingana na uhalisia wa idadi ya watu.
Naye mkaazi wa eneo la Chuo cha Mipango, Judith Malongo amesema kuwa “Ni vizuri kwa wananchi wenzangu kuhakiki anwani zao za makazi kwani inawarahisishia makazi yao kutambulika na kufikishiwa huduma kwa urahisi”. Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na huduma za zima moto, ndugu na jamaa kufika nyumbani kwa urahisi, kufikishiwa bidhaa au huduma mlangoni (Posta Mlangoni).
Aidha, Bi. Malongo amesisitiza kuwa hamasa hii ya uhakiki wa anwani na makazi ambayo inatumia mifumo ya kielektroniki inaenda sambamba na wito wa Serikali wa kuwa na uchumi wa kidijiti.
Kwa upande wake, Mhandisi Mbugi amelizungumzia zoezi la uhakiki la Anwani za Makazi ni mwendelezo wa utekelezaji wa Wizara kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ya kuendesha zoezi hilo na kukamilika ifikapo au kabla ya tarehe 10 Agosti 2022.