Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki Azindua Maduka 31 ya Airtel  :Asema Uwekezaji wa Airtel ni Fursa kwa Vijana na Biashara Ndogo


Na Mwandishi wetu - WMTH Dodoma 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb) amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha Sekta ya Mawasiliano ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Waziri Kairuki ameyasema hayo tarehe 06 Februari, 2026 wakati akizindua maduka 31 mapya ya Airtel Tanzania huku akiongeza kuwa maduka hayo yataongeza upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano, kufungua fursa za ajira hususan kwa vijana, na kukuza biashara ndogo ndogo na za kati zinazotegemea huduma za kidigitali. 

Waziri Kairuki alipongeza Airtel Tanzania kwa uzinduzi wa maduka hayo ya kisasa 31 chini ya kaulimbiu ya “Airtel Kila Kona”, akisema mpango huo unaonesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuwafikia Watanzania walioko kila kona ya nchi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Airtel Tanzania, Bw. Charles Kamoto, alimshukuru Mhe. Waziri kwa kushiriki katika uzinduzi huo na kuendelea kuipa Airtel ushirikiano unaowezesha kampuni hiyo kutekeleza mipango yake ya upanuzi wa huduma. Alisema uzinduzi wa maduka hayo 31 ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kuimarisha ukaribu na wateja pamoja na kuhakikisha huduma za mawasiliano na malipo ya kidigitali zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati.

Bw. Kamoto aliongeza kuwa Airtel Tanzania itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo ujenzi wa minara mipya, ili kuhakikisha Watanzania wanapata mawasiliano ya uhakika na yenye ubora. Alisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kufanikisha ajenda ya taifa ya ujumuishwaji wa kidigitali na maendeleo ya uchumi wa kidigitali.

Naye Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Bi. Adriana Lyamba, alimshukuru Mhe. Kairuki na kueleza kuwa uwepo wake unaonesha dhamira ya Serikali katika kuunga mkono juhudi za sekta binafsi. Alisema Airtel Tanzania imekuwa ikinufaika na ushirikiano mzuri kutoka Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hali inayowezesha kampuni hiyo kuwafikishia wananchi huduma kwa wakati na kwa ufanisi.

Bi. Lyamba alibainisha kuwa maduka hayo mapya ya Airtel ni maduka ya kidigitali (Smart Shops) yasiyotumia karatasi, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma, kupunguza muda wa wateja.

Uzinduzi wa maduka hayo 31 unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ajira kwa vijana kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi wa Dodoma na maeneo mengine.