Habari
WIZARA YA MAWASILIANO YAHITIMISHA ZIARA YA MAANDALIZI YA PROGRAMU YA NDTI KATIKA CHUO KIKUU CHA MUST
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mbeya
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imehitimisha ziara yake katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) inayolenga maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Chuo Mahiri cha Taifa cha TEHAMA (NDTI). Ziara hiyo imefanyika leo, tarehe 04 Februari 2026.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI), Dkt. Ally Simba, amesema kuwa Wizara ipo katika hatua za mwisho za kuleta vifaa vya TEHAMA, na kwamba ziara hiyo imelenga kukagua na kuthibitisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa vifaa hivyo. Ameongeza kuwa maandalizi hayo yanalenga kuanza kwa mafunzo ya TEHAMA katika ngazi za awali na za juu.
Katika ziara hiyo, Timu ya Wizara ya Mawasiliano pia ilipata fursa ya kutembelea majengo yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha MUST kwa ajili ya uwekezaji wa vifaa vya TEHAMA. Wataalam hao walibaini kuwa chuo hicho tayari kimeanza utekelezaji wa programu za ubunifu kupitia Kituo cha Ubunifu na Uhawilishaji wa Teknolojia (Center for Innovation and Technology Transfer – CITT-MUST). Hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa 2050 kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya kukuza ubunifu wa TEHAMA ili kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili jamii.
Akihitimisha ziara hiyo, Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Bakari Mwangugu, ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha MUST kwa ushirikiano waliouonesha na kukipongeza chuo hicho kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika maendeleo ya Teknolojia.
Aidha, amewahimiza vijana wabunifu wa TEHAMA kushiriki katika maonesho makubwa ya kitaifa na kimataifa kama TAIC na AIDA ili kupata fursa za wawekezaji na kuendeleza vipaji vyao.
Lengo la Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI) ni kuongeza ajira kwa vijana, kupunguza pengo la maendeleo ya teknolojia ya kidijitali kati ya Tanzania na mataifa mengine, pamoja na kuongeza vituo vya ubunifu kwa wananchi wenye mawazo ya kiteknolojia.
