Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yafakisha Huduma za Mawasiliano mkoani Tabora


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Bungeni, Dodoma

 

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema imefanikisha kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata sita za Jimbo la Tabora Mjini.

 

Akijibu swali la Mhe. Hawa Subira Mwaifunga (Mbunge wa Tabora Mjini) Bungeni jijini Dodoma leo Februari 06, 2025, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zachari Mkama (Mb) amesema kuwa Kata ya Ikomwa imefikiwa na huduma za Airtel, Vodacom na Halotel; Kata ya Ndevelwa (Halotel); Kata ya Ntalikwa (Airtel); Kata ya Kabila (Honora, Airtel na Halotel); Kata ya Kalunde (Honora, Vodacom, Airtel na Halotel) pamoja na Kata ya Itetemia (Halotel).

Mhe. Dkt. Mkama ameeleza kuwa Kata zote hizo zimejengewa Minara ya Mawasiliano ambayo imekamilika na ipo katika matumizi. Hata hivyo, kutokana na hoja ya Mbunge kuashiria kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo, Wizara kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na Watoa Huduma za Mawasiliano itatuma wataalamu katika Jimbo la Tabora Mjini ili kufanya tathmini ya kina ya hali halisi ya huduma za mawasiliano.

 

Mhe. Dkt. Mkama amefafanua kuwa changamoto za mawasiliano zinaweza kujitokeza hata katika maeneo yenye minara kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu, ukuaji wa shughuli za kiuchumi pamoja na jiografia ya eneo husika. Aidha, kuanzishwa kwa makazi mapya katika maeneo ambayo awali hayakuwa na wakazi kumeongeza mahitaji ya kuboreshwa (optimization) kwa minara iliyopo au kujengwa kwa minara mipya.

Ameongeza kuwa tathmini itakayofanyika itaelekeza suluhisho sahihi, ikiwemo kuongeza nguvu ya mitambo katika minara iliyopo au ujenzi wa minara mipya. Endapo itahitajika kujenga minara mipya, Kata husika zitajumuishwa katika miradi ya Wizara kulingana na upatikanaji wa fedha.

 

Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Mkama amesema kuwa kupitia Mradi wa Awamu ya 11 unaotarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi Februari 2026, Kata ya Ndevelwa, Kijiji cha Itulu, itanufaika na ujenzi wa mnara mpya wa mawasiliano.