Habari
WIZARA YA MAWASILIANO YATOA MAFUNZO YA USALAMA WA MTANDAO KWA WATUMISHI

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma,
Watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamepatiwa mafunzo ya uelewa kuhusu matumizi salama ya mtandao kwa kuchukua tahadhari wanapotumia mtandao kwa matumizi binafsi au kutoa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Oktoba 3, 2025 katika ofisi za Wizara hiyo ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya mwezi wa usalama mtandao yenye kaulimbiu “Baki Salama Mtandaoni”.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa TEHAMA, Bw. Mussa Patrick Chiwelenje, alisema kuwa kila mwezi Oktoba dunia huadhimisha kampeni za usalama wa mtandao.
Alisema maendeleo ya kidijitali yamefungua fursa kubwa kwa jamii lakini pia yameambatana na changamoto za uhalifu wa mtandaoni, utapeli na wizi wa taarifa binafsi.
Bw. Chiwelenje aliwataka watumishi kutumia nywila salama, kulinda watoto mtandaoni na kusambaza taarifa sahihi ili kujenga Tanzania salama ya kidijitali.
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu, Bi. Josephine Mwaijande, alisema mafunzo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Menejimenti ya Ajira kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa watumishi wanapaswa kushirikisha jamii na familia zao maarifa ya usalama wa mtandao badala ya kuyaweka kwa matumizi yao pekee.
Mwanasheria na Msaidizi wa Katibu Mkuu, Bi. Eunice Masigati, aliwasilisha mada kuhusu jitihada za Serikali za kulinda anga la mtandao kwa kutunga Sera ya TEHAMA, kutengeneza mifumo ya usalama, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na kuanzisha tume ya kusimamia ulinzi wa taarifa binafsi.
Alibainisha kuwa Tanzania ipo kwenye hatua za mwisho za kujiunga na Umoja wa Usalama wa Mtandao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (SADC).
Mtaalamu wa TEHAMA, Bw. Hafidhi F. Masoud, alisisitiza kuwa usalama wa mtandao unaanzia kwa mtu binafsi kupitia hatua kama vile kutumia uthibitisho wa utambulisho wa njia mbili na kusasisha na kuzima vifaa baada ya matumizi.