Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YA MAWASILIANO YATOA MAFUNZO YA KIDIGITALI KWA VIJANA KONDOA


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Kondoa

 

Wataalam kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wametoa mafunzo ya matumizi ya mifumo ya kidigitali kwa vijana wa Wilaya ya Kondoa, kwa lengo la kuwawezesha kupata huduma mbalimbali za serikali pamoja na kujiongezea kipato kupitia teknolojia.

 

Mafunzo hayo yametolewa Juni 2, 2026, kwenye Kongamano la Vijana lililofanyika katika Shule ya Sekondari Aman Abeid Karume, iliyopo Kijiji cha Pahi, Wilaya ya Kondoa.

 

Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Halidi Nyange, amesema kuwa huduma nyingi kwa sasa zinapatikana kwa njia ya kidigitali, hivyo ni muhimu kwa Vijana kujifunza na kutumia mifumo hiyo ili kunufaika na fursa zilizopo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini.

 

Aidha ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidigitali yamerahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali, ikiwemo kuomba nafasi za masomo ya Elimu ya juu, kufanya malipo ya serikali, kupata leseni za biashara, kutengeneza maudhui ya kuelimisha jamii pamoja na huduma nyingine muhimu. Ambapo mpaka sasa asilimia 50 ya wananchi wananufaika na huduma kupitia mifumo hiyo, Jambo linaloonesha kuimarika kwa mazingira ya uchumi wa Kidigitali.

 

Kwa upande mwingine, Bw. Nyange amesema Serikali inaendelea kuboresha na kuunganisha mifumo ya utoaji huduma ili iweze kusomana, hatua inayolenga kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

 

Pia amewahimiza vijana kujiwekea malengo yatakayowawezesha kumiliki vifaa vya kidigitali kama simu janja na kompyuta, pamoja na kutumia intaneti kwa manufaa ya kujifunza, kuendeleza ujuzi wa kidigitali, kuanzisha biashara mtandaoni na kubuni fursa mpya za kiuchumi.

 

Katika kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya mifumo kusomana, Bw. Nyange ameeleza kuwa, Wizara imeandaa Mkakati wa Tanzania Technology Stack (Jamii Stack) unaolenga kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga jamii ya kidigitali na kuhakikisha mifumo ya Mawasiliano na utoaji huduma inasomana kwa ufanisi.

 

Katika hatua nyingine,  amewataka vijana kuzingatia usalama mtandaoni kwa kuepuka kutoa taarifa binafsi bila tahadhari, kutofungua viunganishi (links) visivyoaminika na kutumia mifumo salama wanapofanya shughuli zao za kidigitali.

 

Amesisitiza kuwa matumizi salama ya teknolojia ni muhimu katika kulinda taarifa za watumiaji na kujenga mazingira bora ya matumizi ya mifumo ya kidigitali nchini.