Habari
WIZARA YA MAWASILIANO YATEMBELEA UDSM KWA MAANDALIZI YA PROGRAMU ZA NDTI
Na Mwandishi Wetu - WMTH, Dar es Salaam.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) ikiwa ni ziara ya kutathmini miundombinu iliyopo itakayowezesha mafunzo ya awali ya umahiri katika Teknolojia za Kisasa.
Akizungumza wakati wa ziara tarehe 30 Januari, 2026 Mkurugenzi wa Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI), Dkt. Ally Simba, alisema ziara hiyo inalenga kufanya maandalizi ya uwekaji wa vifaa vya TEHAMA vitakavyotumika katika mafunzo ya awali yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni chuoni hapo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya CoICT, Prof. Baraka Jakob Maiseli, alieleza utayari wa chuo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo ya teknolojia na ujuzi wa kidijitali.
Naye Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali , Bw. Bakari Mwangugu alisema kuwa mitaala ya mafunzo hayo imeandaliwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DTI) huku UDSM ikiteuliwa kuwa mshauri elekezi wa mradi ili kuhakikisha ubora wa mafunzo yatakayotolewa.
Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI) unatarajiwa kuchangia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana na kuchochea uanzishaji wa kampuni bunifu, ambapo uongozi wa CoICT umeeleza kuwa chuo kipo tayari kwa miundombinu na rasilimali watu zitakazohitajika katika utekelezaji wa mradi huo.
