Habari
Wizara ya Mawasiliano Yasisitiza Uchumi wa Kidijitali kwa Wajasiriamali Wadogo na Wakati
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Arusha
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), amehimiza wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) kutumia teknolojia za kidijitali ili kuongeza ufanisi, kujenga uwezo na kupanua fursa za kibiashara.
Mhe. Dkt. Mkama ametoa kauli hiyo katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kwa Wajasilimali Wadogo na wa Kati lililofanyika tarehe 18 Aprili 2026 jijini Arusha.
Kongamano hilo lilifunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ambapo jumla ya wajasiriamali 45 walitunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo ya biashara yaliyotolewa na Taasisi ya KLI.
Kongamano hilo liliandaliwa na Asasi ya Kiraia ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT-KLI) kwa kushirikiana na Regent University (RCE) kutoka Marekani pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kupitia Tume ya TEHAMA imeahidi kushirikiana na KLNT kuanzisha na kuendeleza Kituo Atamizi cha Kidijitali (Digital Incubation Hub) kwa lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali hao na kuwasaidia kukuza biashara zao.
