Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tanzania Yaahidi Kuendeleza Mageuzi ya Kidijitali na Ushirikiano wa Afrika.


Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU Conference of Plenipotentiaries – CPL-26), jukwaa ambalo huwakutanisha viongozi wa Sekta ya Mawasiliano kutoka nchi wanachama wa Afrika kujadili mustakabali wa mawasiliano na teknolojia za kidijitali barani.

Akihutubia katika mkutano huo, Mhe. Dkt. Mkama aliwasilisha mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika kipindi cha miaka minne iliyopita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa huduma za TEHAMA, kuimarisha uchumi wa kidijitali na kusogeza huduma za serikali karibu zaidi na wananchi kupitia teknolojia.

Aidha, Mhe. Dkt. Mkama alisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na nchi nyingine za Afrika kupitia Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU) katika kujenga sera, mifumo na uwekezaji utakaoharakisha mageuzi ya kidijitali, kupunguza pengo la kidijitali na kuhakikisha teknolojia inakuwa chachu ya maendeleo jumuishi na endelevu barani Afrika.

Ushiriki wa Tanzania katika ATU CPL-26 unaonesha dhamira ya nchi kuendelea kuwa mshirika muhimu katika kuunda mustakabali wa sekta ya mawasiliano na TEHAMA Afrika, sambamba na kuchangia ajenda ya bara ya uchumi wa kidijitali na maendeleo ya jamii kupitia matumizi ya teknolojia.

#ATUCPL26 #DigitalTransformation #ICT #DigitalEconomy #Tanzania #Africa #Connectivity #Innovation