Habari
TANZANIA YASHINDA NAFASI YA MJUMBE WA BARAZA LA UTAWALA LA UMOJA WA MAWASILIANO AFRIKA (ATU)
Na Mwandishi Wetu, Abuja, Nigeria
Tanzania imechaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Utawala la Umoja wa Mawasiliano Afrika (African Telecommunications Union – ATU), hatua inayodhihirisha imani ya nchi wanachama kwa mchango wa Tanzania katika kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) barani Afrika.
Uchaguzi huo ulifanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU Conference of Plenipotentiaries – CPL-26) uliofanyika tarehe 24 Julai, 2026 jijini Abuja, Nigeria, na kuwakutanisha wajumbe kutoka nchi 54 wanachama wa ATU. Kati ya nchi hizo, ni nchi 25 pekee zilizochaguliwa kuunda Baraza la Utawala la umoja huo kwa kipindi kijacho.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), ambaye aliwakilisha nchi katika majadiliano na maamuzi mbalimbali ya kimkakati yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuendeleza miundombinu ya mawasiliano, kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali na kukuza uchumi wa kidijitali barani Afrika.
Kuchaguliwa kwa Tanzania katika Baraza la Utawala la ATU kunaipa nchi nafasi muhimu ya kushiriki katika maamuzi ya sera na mwelekeo wa maendeleo ya sekta ya mawasiliano Afrika, sambamba na kuendeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali na kuhakikisha Watanzania wanapata manufaa zaidi kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Mbali na uchaguzi wa Baraza la Utawala, mkutano huo pia ulifanya uchaguzi wa Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU), ambaye ataongoza utekelezaji wa mipango na maamuzi ya umoja huo katika kipindi kijacho.
#ATUCPL26 #DigitalTransformation #ICT #DigitalEconomy #Tanzania #Africa #Connectivity #Innovation
