Habari
SERIKALI YAKAMILISHA UJENZI WA MKONGO WA TAIFA TABORA–MPANDA.
Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Tabora hadi Mpanda kupitia Sikonge, Ipole na Inyonga, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na intaneti yenye kasi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati akijibu swali la Mhe. Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaweka Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kijiji cha Ipole, Wilaya ya Tabora, hadi Kata ya Inyonga, Wilaya ya Mlele, kutokana na changamoto ya uwepo wa wanyama wakali katika eneo hilo.
Mhe. Dkt. Mkama amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unafika katika wilaya mbalimbali nchini, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma za intaneti yenye kasi na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Ameeleza kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaunganishwa na miundombinu ya watoa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini, hatua inayowezesha huduma za mawasiliano na intaneti kuwafikia wananchi katika maeneo yanayounganishwa na mkongo huo.
Aidha, Naibu Waziri Mkama amesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/26, Serikali imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Tabora hadi Mpanda kupitia Sikonge, Ipole na Inyonga. Amesema mkongo huo umejengwa kwa kutumia miundombinu ya umeme ya TANESCO, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuwaunganisha watoa huduma za mawasiliano katika maeneo hayo ili waweze kuwafikishia wananchi huduma za mawasiliano na intaneti.
