Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUIMARISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO KILIMARONDO NA KIEGEI.


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Bungeni, Dodoma.

Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Kata za Kilimarondo na Kiegei katika Jimbo la Nachingwea, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma muhimu za mawasiliano na fedha kwa urahisi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), wakati akijibu Swali la Mbunge wa Nachingwea, Mhe. Fadhili Ally Liwaka, aliyetaka kujua ni lini huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zitawafikia wananchi wa Kilimarondo na Kiegei ambao kwa sasa hulazimika kusafiri umbali wa takriban kilometa 120 kufuata huduma hiyo.

Mhe. Dkt. Mkama amemwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapatiwa huduma za kifedha kupitia mtandao wa TTCL, (T- Pesa) kwa kuwa tayari huduma za mawasiliano za TTCL zinapatikana katika maeneo hayo.

Aidha, amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini ya changamoto za mawasiliano katika maeneo ya Kilimarondo na Kiegei, kwa lengo la kubaini mahitaji yaliyopo na kuwezesha kuongezwa kwa watoa huduma wengine wa Mawasiliano.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa jimbo la Bunda Mjini, Mhe. Ester Bulaya, kuhusu ujenzi wa minara katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano jimboni kwake, Mhe. Dkt. Mkama amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto hizo kwa kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo husika, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya kuimarisha mawasiliano nchini katika mwaka wa fedha 2026/2027.