Habari
TANZANIA YAWEKA MIKAKATI YA KUJENGA MAWASILIANO JUMUISHI YA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu
Nassau, Bahamas
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano zilizo jumuishi, nafuu, salama na zenye uhakika, sambamba na kuimarisha ujuzi wa kidijitali na matumizi yenye tija ya teknolojia.
Waziri Kairuki ameyasema hayo wakati akishiriki Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Sera za Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (WTPF-26), unaofanyika jijini Nassau, Bahamas, ambapo amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zinalenga kutekeleza kwa vitendo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024–2034.
Mkutano wa Saba wa WTPF-26, unaofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 4 Septemba 2026, umebeba kaulimbiu “Kuharakisha Mustakabali wa Kidijitali Jumuishi, Endelevu, Imara na Bunifu,” na unawakutanisha viongozi, watunga sera, wataalamu na wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani kujadili masuala muhimu ya sera yanayohusu mustakabali wa mawasiliano na TEHAMA.
Akizungumza katika moja ya mijadala ya Jukwaa hilo, Waziri Kairuki amesema kuwa, Tanzania imekamilisha ujenzi wa minara 758 ya teknolojia ya 4G, iliyowezesha zaidi ya vijiji 1,400 na takribani wananchi milioni 8.5 waliokuwa hawapati huduma za mawasiliano ya uhakika kuunganishwa na huduma hizo.
Aidha, amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutekeleza hatua za kuongeza matumizi jumuishi ya teknolojia, ikiwemo kuanzisha Vilabu vya Kidijitali 800 kwa ajili ya kujenga ujuzi wa TEHAMA, kuwezesha upatikanaji wa huduma za Wi-Fi katika maeneo 100 ya umma, pamoja na kujenga maabara za kompyuta katika shule 250 za umma, zikiwemo huduma zinazozingatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.
Akieleza msimamo wa Tanzania katika juhudi za kimataifa za kuziba pengo la kidijitali, Waziri Kairuki amesema Tanzania inapendekeza maeneo matatu ya kipaumbele, ambayo ni kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu; kuongeza ujuzi wa kidijitali na matumizi ya Akili Unde (AI) kwa makundi mbalimbali ya jamii; na kuendeleza miundombinu ya kidijitali iliyo salama, jumuishi na inayolinda taarifa binafsi za watumiaji.
Waziri Kairuki amesema kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) za mwaka 2025, takribani watu bilioni 2.2 duniani bado hawajaunganishwa na intaneti, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kupanua huduma za kidijitali, hususan kwa jamii ambazo hazijafikiwa kikamilifu.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na ITU pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika kuimarisha ujuzi wa kidijitali na matumizi ya Akili Unde barani Afrika, hususan katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini, ili kuhakikisha mapinduzi ya kidijitali yanawanufaisha wananchi wengi zaidi na kuchochea maendeleo jumuishi.
“Mafanikio katika mageuzi ya kidijitali hayapaswi kupimwa kwa idadi ya minara iliyojengwa pekee, bali kwa namna teknolojia inavyoboresha maisha ya wananchi, kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii, na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika uchumi wa kidijitali,” amesema Waziri Kairuki.
Mkutano wa Saba wa WTPF-26 unatoa fursa kwa nchi wanachama wa ITU kubadilishana uzoefu na mitazamo kuhusu maeneo muhimu yakiwemo kuziba pengo la kidijitali, kuimarisha uhimilivu wa miundombinu ya mawasiliano, kukuza muunganisho kupitia teknolojia za anga za juu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mageuzi ya kidijitali, pamoja na kuimarisha mifumo ikolojia ya ubunifu na ujasiriamali katika sekta ya TEHAMA.
