Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YA MAWASILIANO YASHIRIKI MAADHIMISHO YA 22 YA SIKU YA WAHANDISI TANZANIA


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Wahandisi 23 kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wameshiriki katika uzinduzi wa Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Tanzania, yaliyoandaliwa na Bodi ya Wahandisi Tanzania (ERB) na kufanyika leo, Septemba 25, 2025, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo, yaliyofunguliwa rasmi na Mhe. Dotto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, yamebeba dhima ya kuangazia nafasi ya wahandisi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2025 na maandalizi ya safari ya kuelekea Dira 2050.

Akihutubia wahandisi na wadau wa sekta hiyo, Mhe. Biteko aliwapongeza wahandisi kwa mchango wao katika ujenzi wa Taifa na kusisitiza kuwa dunia ya sasa inategemea sekta ya uhandisi kama mhimili wa maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ERB, Mhandisi Menye Manga, amesema taaluma ya Uhandisi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kidijiti nchini. Aidha, aliwataka wahandisi wapya kuhakikisha wanajisajili kupitia mfumo mpya wa kidijiti wa ERB uliyozinduliwa rasmi na Mhe. Biteko.

Aidha, mbali na kushiriki katika mijadala na mafunzo, Wizara ya Mawasiliano na TEHAMA imeshiriki pia kwenye mabanda ya maonesho, ambapo wataalam wake wameendelea kutoa elimu kuhusu mifumo ya TEHAMA na mchango wake katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijiti na kukuza uchumi wa kidijiti wa taifa.

Katika maadhimisho hayo, Mhandisi Stephen Wangwe kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), taasisi iliyo chini ya Wizara, alitoa mada kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi. Alisisitiza kuwa taarifa binafsi zinapaswa kushughulikiwa kwa namna inayoheshimu haki na faragha za wananchi, huku akitoa wito kwa jamii kuhakikisha inalinda taarifa zake binafsi dhidi ya matumizi mabaya.