Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YA MAWASILIANO YAPONGEZWA KWA USHIRIKIANO UHAKIKI ANWANI ZA MAKAZI SONGEA


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Songea

Mtendaji wa Kata ya Lizaboni, Halmashauri ya Songea, Bi. Kissa Lusekelo Brown, amepongeza ushirikiano unaotolewa na wataalam wa mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Halmashauri hiyo, akisema msaada wao umekuwa chachu ya mafanikio katika zoezi la uhakiki wa taarifa za anwani.

Akizungumza Septemba 28, 2025, ofisini kwake katika Mtaa wa Polisi, Jengo Namba 9, Lizaboni,  Songea, Bi. Kissa alisema wataalamu hao wamekuwa msaada mkubwa hasa pale changamoto zinapojitokeza.

Aidha, aliwataka watendaji na wananchi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na kuleta tija kwa maendeleo ya jamii.

Bi. Kissa alifafanua kuwa lengo kuu la uhakiki huo ni kusasisha taarifa mpya zinazojitokeza kila siku kutokana na ukuaji wa makazi na ongezeko la wananchi.

Akieleza faida za mfumo huo, alitaja miongoni mwa manufaa yake kuwa ni urahisi wa utambuzi na ufikishaji wa huduma muhimu, ikiwemo usambazaji wa vifurushi kupitia Shirika la Posta Tanzania.