Habari
WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI YAKAGUA VITUO VYA UBUNIFU KATIKA CHUO CHA MUST IKIWA NI UTEKELEZAJI WA MRADI WA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA (NDTI)
Na Mwandishi wetu-WMTH, Mbeya
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST). Ziara hii imelenga kutembelea vyuo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye maeneo ya ubunifu ikiwa ni matayarisho ya uanzishaji wa Chuo Mahiri Cha TEHAMA kitakachojengwa katika eneo la Nala, Mkoani Dodoma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Mifumo, Huduma za TEHAMA na Uzingatiaji kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohamed Mashaka, amesema Wizara ipo katika hatua za uanzishaji wa vituo vya ubunifu katika chuo hicho na hivyo ziara hii ni katika kuangalia utayari wa maeneo haya ya ubunifu ambayo Wizara itayaanzisha kwa kushirikiana na vyuo mbalimbali ikiwemo MUST.
Bw. Mashaka alieleza kuwa Wizara inashirikiana na vyuo mbalimbali vya Teknolojia nchini katika kuhakikisha Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa kidijitali wa mwaka 2024/34, na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kupitia jitihada za kukuza matumizi ya TEHAMA, unaimarisha ubunifu na kutafuta suluhisho za changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwa kutumia teknolojia.
Wataalamu hao pia walijionea utekelezaji wa programu mbalimbali za ubunifu kupitia Kituo cha Ubunifu na Uhawilishaji wa Teknolojia (Center for Innovation and Technology Transfer – CITT-MUST), hatua inayodhihirisha utayari wa chuo hicho katika kukuza ubunifu wa kidijitali Nchini.
Kwa upande wake, Prof. Zacharia Katambara, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) amesema kuwa chuo kipo tayari kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika maeneo ya kukuza ubunifu wa vijana wa kitanzania na alipongeza jitihada za Wizara zinazoendelea katika uanzishaji wa Chuo Mahiri cha TEHAMA.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo na huduma za TEHAMA na Uzingatiaji ambae pia ni Mratibu wa NDTI, Dkt. Angelina Misso ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha MUST kwa ushirikiano waliouonesha na kukipongeza chuo hicho kwa jitihada inazozifanya na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika maendeleo ya teknolojia na ubunifu nchini na kuweka mazingira wezeshi kwa vijana.
