Habari
WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI YAENDELEA NA MAANDALIZI YA UANZISHAJI WA PROGRAMU ZA NDTI SUZA
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Zanzibar
Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI), Dkt. Ally Simba, leo imefanya kikao kazi na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa lengo la kujadili maandalizi ya uwekaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) chuoni hapo.
Timu hiyo ilipokelewa na Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Abdi Talib Abdallah, ambaye aliipongeza Wizara kwa kutembelea chuo hicho na kwa kukipa kipaumbele katika utekelezaji wa Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI).
Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Abdi Talib alisema kuwa uongozi wa SUZA uko tayari kushirikiana kikamilifu na Wizara ili kuhakikisha maandalizi yote yanatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa mipango iliyowekwa. Pia, aliahidi kuwa chuo kitahakikisha utekelezaji wa mradi huo unakwenda kama ilivyopangwa.
Katika ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo aliwaonesha wajumbe wa timu ya Wizara eneo lililotengwa kwa ajili ya maabara ya TEHAMA, akibainisha kuwa eneo hilo lina ukubwa wa kutosha pamoja na mazingira rafiki yatakayowezesha usimikaji wa vifaa vya kisasa vya TEHAMA mara vitakapowasili chuoni hapo.
Kwa upande wake, Dkt. Ally Simba alisema kuwa ziara hiyo imelenga kufanya tathmini ya awali ya miundombinu ya chuo kwa ajili ya uwekaji wa vifaa vya TEHAMA vitakavyotumika katika uanzishaji wa programu za awali za mafunzo ya NDTI, ambazo zinatarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, hatua inayotarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga uwezo wa vijana katika teknolojia za kidijitali na kuendeleza ajenda ya uchumi wa kidijitali nchini.
