Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YA HABARI YAWEKA MKAZO USIMAMIZI WA VIHATARISHI


Wataalamu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wametakiwa kuhakikisha wanakuwa chachu ya kuboresha mfumo wa usimamizi wa vihatarishi (Risk Management Framework) na kuleta matokeo chanya kwa Wizara.

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano, Bw. Mulembwa Munaku alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na kufungua kikao kazi cha siku tano kwa wataalamu hao yanayofanyika jijini Arusha kwa lengo la kuhuisha daftari la vihatarishi (Risk register) kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Kikao kazi hiki kiwe chachu ya kuboresha zaidi mfumo wa usimamizi wa vihatarishi na kuleta matokeo chanya katika malengo tuliyojiwekea hususani kwenye miradi ya kisekta ili kuhakikisha inatekelezwa kwa umakini na ubora stahiki”, amesisitiza Munaku

Aidha, Munaku ametoa rai kwa wataalamu hao kuhakikisha wanahuisha daftari la vihatarishi kwa kubainisha uhalisia wa vihatarishi, kuvichambua upya na kuvipa uzito, kubaini vihatarishi vipya na kuandaa mipango madhubuti wa kudhibiti na kushughulikia vihatarishi hivyo.

Katika hatua nyingine, Bw. Munaku amempongeza Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Wizara hiyo, CPA, Joyce Christopher kwa kazi nzuri kuhakikisha udhibiti wa vihatarishi unafanyika ili kutokwamisha jitihada za Serikali  katika Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

“Tukiwa kama taasisi ya umma tunatakiwa kuwajibika na kusimamia kwa umakini mkubwa vihatarishi vitavyoainishwa na kuvishughulikia, utekelezaji huo uwe shirikishi na ufuate sera, sheria, taratibu na miongozo inayosimamia sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari”, amesisitiza Munaku.

Naye, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Wizara hiyo, CPA, Joyce Christopher amesema kwa miaka mitatu mfululizo toka mwaka 2020 Wizara imekuwa ikiandaa mfumo mahsusi wa kushughulikia vihatarishi kwa kuandaa mpango kazi na rejesta ya vihatarishi na taarifa za utekelezaji wake zimekuwa zikiwasilishwa kwenye Menejimenti na Kamati ya Ukaguzi ya Wizara.

“Tumekuwa tukisifiwa na Kamati ya Ukaguzi kwa kuandaa mfumo Madhubuti wa kushughulikia vihatarishi, jitihada za pamoja baina ya wataalamu na menejimenti ya Wizara zinasaidia  katika uandaaji, usimamizi na  mapitio ya utekelzaji wa Rejesta ya Usimamizi wa Vihatarishi”, amesema Christopher.